Ulanga
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mh. Jacob Kassema amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya kuanzisha siku ya familia kwa watumishi wa Halmashauri yake.
Aliyasema hayo wakati wa sherehe za bonanza la walimu lililofanyika Wilayani Ulanga kwa kuwakutanisha walimu wa shule za Sekondari na Msingi na kucheza michezo mbalimbali katika uwanja wa Mapinduzi na ukumbi wa Udeco.
Alifafanua kuwa siku hiyo ina umuhimu sana kwa ajili ya kujenga mahusiano kati ya watoto wa Mkuu wa Idara moja na mwingine na unajenga mshikamano kwa kizazi cha sasa na kijacho na kinyume na hapo ni kujenga kizazi cha watu wasiojuana na kutokuwa na umoja.
Aliongeza kuwa katika bonanza hilo ameona vipaji mbalimbali vya walimu ambavyo vikitumika vizuri vinaweza kutumika katika kuwajenga wanafunzi kisanii na baadae wakajiajili wenyewe na mbali na kuonyesha vipaji walimu wamepata kujumuika na kusahau shida zinazowakabili na kufanya wajione wenye thamani katika jamii.
Akitaja malengo ya tamasha hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Yusuf Semuguruka amesema walimu wengi wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo tofauti hivyo kwa kuwakutanisha katika tamasha hilo kumeleta umoja na afya kutokana na michezo mingi iliyochezwa katika siku hiyo.
Aidha aliongeza kuwa tamasha hilo lilifanyika mahsusi kwa ajili ya kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa akipenda michezo hivyo kwa kushirikiana na Chama Cha Walimu Wilaya wakaona ni bora kufanya bonanza hilo ili kuwakutanisha walimu hao.
Bonanza la walimu lilifanyika hivi karibuni Wilayani Ulanga na kufana kwa kiasi kikubwa ambapo walimu wengi walihudhuria tamasha hilo kwa kucheza michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, mpira wa pete, mpira wa miguu, mpira wa wavu, kukimbiza kuku, kukimbia kwenye magunia na kufuatiwa na disco la walimu walioimba nyimbo mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.