ULANGA
NA Fatuma Mtemangani
Kamishna jenerali wa Magereza Afande Phaustine Kasike amefanya ziara ya kihistoria katika gereza la Mahenge Wilayani Ulanga mkoani Morogoro na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na gereza hilo.
Kamishna Jenerali Afande Kasike alipokelewa na mkuu wa gereza la Mahenge Afande Stockwell Mlyuka na kusomewa taarifa fupi ya kituo hicho na pia alipata nafasi ya kuongea na wafungwa pamoja na mahabusu wa gereza hilo ili kusikiliza shida na kero mbalimbali zinazowakabili.
Kamishna jenerali alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo zahanati,nyumba ya kufikia askari wageni[Rest House]hasa wanaotoka mafunzoni[Depo],Mabwawa ya samaki aina ya sato pamoja na uzalishaji wa Mifugo .
Pia kamishna jenerali amempongeza mkuu wa gereza la Mahenge Afande Stockwell Mlyuka kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo na kumtaka aendelee kubuni miradi mingine itakayosaidia jeshi na Taifa kwa ujumla kwani jeshi la gagereza lipo katika mpango wa kujitegemea hasa kwa upande wa chakula.
Hata hivyo kamishna jenerali Kasike alipata nafasi ya kuzungumza na maafisa na askari wa gereza hilo na kufurahia kuona wanafanya kazi kwa ushirikiano hivyo amewataka watumishi hao kuendeleza ushirikiano huo kwa mkuu wa gereza hilo kwa ajili ya kuleta maendeleo na pia kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa bidii,maarifa na weledi na kufuata kanuni na taratibu za jeshi la magereza japo kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili jeshi la magereza tayari baadhi ya changamoto hizo zimeanza kupatiwa ufumbuzi.
“Nimefurahi sana kuona mnafanya kazi kwa kushirkikiana vizuri najua kuna changamoto nyingi zinawakabili jeshi la Magereza lakini kwa sasa baadhi ya changamoto hizo zinafanyiwa ufumbuzi na zingine zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi hivyo mnapaswa kufanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za jeshi la Magereza na muache kufanya kazi kwa mazoea.”Alisema kamishna jenerali Kasike.
Aidha amewataka watumishi wa jeshi la Mgereza Mahenge kujiepusha na vitendo vya kupokea au kutoa rushwa na yeyote atakaebainika anafanya vitendo hivyo kinyume na maadili ya jeshi la magereza atachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwa na kufukuzwa kazi.
Kwa upande wake mkuu wa gereza hilo Afande Stockwell Mlyuka amemuahidi kamishna jenerali Kasike kutomuangusha na ataendelea kufanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za jeshi la magereza hivyo hatomuonea aibu asakari yeyote atakaekiuka maadili ya jeshi la magereza,pia kuendelea kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo katika gereza hilo.
Katika ziara hiyo kamishna jenerali Kasike aliongozana na kamanda wa magereza wa mkoa wa Morogoro afande Silvester Mrema pamoja na maofisa wengine wa jeshi la magereza.
Kamishna jenerali Phaustine Kasike ameahidi kutembelea vituo vyote vilivyo pembezoni ikiwemo gereza la Mahenge ambapo Kumbukumbu za gereza hilo zinaonesha kuwa halikuwahi kutembelewa na mkuu wa jeshi la magereza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1886 hivyo ziara ya kamishna jenerali Kasike imekuwa ni ya kihistoria katika gereza la Mahenge lililopo Wilayani Ulanga mkoani Morogoro.
Mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.