ULANGA
Na
Fatuma Mtemangani
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesimamisha shughuli za uchimbaji madini ya kinywe na vito katika machimbo ya Epanko yaliyopo katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro ili Serikali iweke kwanza utaratibu mzuri wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo kabla ya kuruhusu uchimbaji madini kuendelea.
Biteko alitoa agizo hilo tarehe 10 Julai, 2018 kwenye ziara yake aliyoifanya katika machimbo hayo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Kamati iliyoundwa na Tume ya Madini kwa ajili ya kuchunguza shughuli za uchimbaji madini katika machimbo hayo.
Hivi karibuni, Naibu Waziri Biteko alielekeza Tume ya Madini kuunda kamati hiyo kwa ajili ya uchunguzi huo na kuwasilisha taarifa yenye mapendekezo ya namna ya kuboresha uchimbaji katika machimbo ya Epanko.
Naibu Waziri Biteko mara baada ya kutembelea eneo hilo na kushuhudia shughuli za uchimbaji madini zikiendelea pasipo kufuata kanuni za mazingira huku katika baadhi ya maeneo mitambo ikiwa imefungwa kwa ajili ya kuondolewa, aliagiza wamiliki wa leseni kukusanya vifaa vya uchimbaji madini chini ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kusimamisha shughuli za uchimbaji madini ndani ya siku tatu hadi Serikali itakapojiridhisha juu ya mwenendo wa shughuli za uchimbaji madini.
Aliendelea kusema kuwa, katika eneo hilo kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria na kanuni za mazingira kwa kuchepusha mto Kilombero hali iliyopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira
Alisema kuwa wachimbaji madini wamekuwa wakitiririsha maji machafu kutoka migodini kwenda kwenye mto Kilombero ambao ni tegemeo kubwa la wananchi wanaozunguka eneo la Epanko jambo ambalo linahatarisha afya zao.
Alisisitiza kuwa wachimbaji madini wengi wamekuwa wakiendesha shughuli zao pasipo kuwa na vibali vya mazingira kama sheria na kanuni za uchimbaji madini zinavyowataka.
Aliongeza kuwa kumekuwepo na changamoto ya kutokuwepo kwa uwazi katika mikataba kati ya wamiliki wa leseni na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini, mapato na kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa serikalini.
Kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya wamiliki wenye leseni kudhulumiwa haki zao na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini na kusisitiza kuwa ni vyema Serikali ikasitisha shughuli zote za uchimbaji madini katika eneo la Epanko na kuanza ukaguzi wa leseni moja moja ili kuona kama zinakidhi sheria na kanuni za madini kabla ya kuruhusu shughuli za uchimbaji madini kuendelea.
Katika hatua nyingine, Biteko alielekeza uanzishwaji wa Ofisi ya Madini katika wilaya ya Ulanga itakayosimamia kwa karibu mwenendo wa shughuli za uchimbaji madini katika wilaya hiyo.
Awali akitoa taarifa ya kamati iliyoundwa kwa ajili ya uchunguzi wa shughuli za uchimbaji madini ya kinywe na vito katika machimbo ya Epanko, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukran Manya alisema kuwa kamati hiyo ilibaini kuwa uchimbaji madini katika eneo hilo ulikuwa hauzingatii sheria na kanuni za madini pamoja na mazingira na kutokuwepo kwa uwazi katika mapato na matumizi katika migodi.
Aliongeza kuwa kamati ilibaini kutokuwepo kwa mikataba kati ya wamiliki wa leseni za madini na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini zilizosajiliwa kwenye Ofisi za Madini na Halmashauri hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro ya mara kwa mara.
Alitaja wachimbaji wanaofanya kazi katika eneo la Epanko kuwa ni pamoja na Peter Chamtitu, Jonas Mpanduli, Sabinus Chigumbi, Franone & Gems na Paskali Jonas Mpanduli & Partners ambao wamelipa mrabaha hadi sasa.
Alitaja wachimbaji wengine ambao hawajalipa mrabaha mpaka sasa kuwa ni pamoja na Mathias Osward Lunkombe & Partners, John Joseph Ntoga na Protas Osward Lunkombe, Moshi Saidi Nassoro na Christoms Martin Msakamba na Bonifas Julai.
Wachimbaji wengine ambao hawajalipa mrabaha ni Joseph Kabu Mworia, John Joseph Ntoga na Franone Mining & Gems Co. Ltd, Joseph Paulo Mwangu & Partners, Mohamedi Said Magonga & Partners, Interstate Mining Limited na Flora Amadei Lyaupe & Partners.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.