Wananchi wa wilaya ya Ulanga wametakiwa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF) ili waweze kupata huduma kwenye vituo vyote vya serikali katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Shinyanga
Akizungumza katika kikao hicho Meneja (CHF) wilayani humo Bi Sigilinda Mdemu alisema kuwa kwasasa huduma zake zimeboreshwa ukilinganisha na miaka iliyopita ambayo mwanachama alikuwa anapata huduma katika eneo alilojiandikisha tu pekee ambapo kwa sasa mwanachama anaweza kupata huduma hiyo katika mikoa mitatu tofauti.
Aidha ameeleza kuwa kwasasa mwanachama ambaye anataka kujiunga anapaswa kuchangia kiasi cha shilingi elfu kumi itakayomwezesha mwanachama na watu wasiozidi sita kupata huduma zote za afya ikiwemo kumwona daktari, vipimo na dawa ikiwa na lengo la kusogeza huduma bora za afya kwa wanachi wote.
Hata hivyo Bi mdemu aliongeza kuwa mfuko wa afya ya jamii (CHF) ipo nje ya fedha ya kapu la pamoja la serikali na kuongeza kuwa uwingi wa wanachama unasaidia kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa madawa kwani serikali hutoa fedha zingine sawa na kiwango kilichokusanywa na kufanya vituo vya afya na zahanati kuagiza madawa zaidi.
Hata hivyo ametoa wito kwa serikali za vijiji kuendelea kuwaelimisha wananchi wao na kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Zaidi ya wadau 50 wakiwemo viongozi mbalimbali wa serikali wilayani Ulanga walikutana na kujadili mikakati mbalimbali ya kuongeza idadi ya wanachama watakaojiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF) ambapo walitoa mbinu mbalimbali za kuboresha mfuko huo na kuandaa mpango mkakati wa uhamasishaji.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.