Ulanga
Na Fatuma Mtemangani
Mkurugenzi mtendaji wa halamashauri ya wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro Ndg Yusuph Semuguruka amefanya ziara katika kituo cha afya Mwaya ili kujionea utendaji wa kazi wa watumishi pamoja na changamoto zinazokikabili kituo hicho.
Semguruka amejionea utendaji wa kazi wa watumishi hao na kujihakikishia uwepo wa madawa na vifaa tiba vilivyoagizwa kituoni hapo kwa lengo la kuondosha kero ya muda kwa wananchi wanaofika kituo cha afya kwa ajili ya huduma za afya.
Baada ya kujionea uwepo wa vifaa tiba mkurugenzi amewataka watumishi hao wa afya kuzingatia maadili ya kazi yao ili kuondosha malalamiko yanayotolewa dhidi yao ikiwemo lugha zisizostahili kwa wagonjwa pamoja na ubadhilifu wa dawa zinazotolewa na Serikali.
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa Kituo cha afya Venance David amemuhakikishia mkurugenzi kuwa kila mtumishi wa kituo hicho anatimiza wajibu wake huku akisisitiza kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na taratibu za utumishi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha amesema changamoto mbalimbali zilizokuwa zikikikabili kituo hicho tayari zimeshughulikiwa zikiwamo zile zilizokuwa zikihusu mfuko wa bima ya afya {CHF} iliyoboreshwa ambazo kwa kiasi kikubwa zililenga upungufu wa dawa na huduma zisizoridhisha kwa wanachma waliojiunga na mfuko huo.
Kituo cha afya mwaya ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vifaa tiba hali iliyowalazimu wagonjwa wanaofika kupata huduma kituoni hapo kununua dawa katika maduka ya watu binafsi na kuibua malalamiko ya huduma kituoni hapo.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Anwani ya Posta: P.O. BOX 22
Telephone: +2550232626340
Simu: 0763845957
Barua pepe: ded@ulangadc.go.tz
Copyright ©2017 Ulanga District Council . All rights reserved.